Mpango wa kubadilishana wanafunzi na GreenVit Imechapishwa mnamo October 15, 2026 8 dakika za kusoma

Wanafunzi wawili wa udaktari kutoka Ujerumani wakiwa na GreenVit Health kwa wiki moja katika afya ya jamii huko Moshi.

sisi GreenVit tulipata bahati ya kuwa wenyeji wa wanafunzi wawili wa udaktari kutoka ujerumani, kwa muda wa wiki moja ya afya ya jamii huko Moshi, haya ndio maoni walikua nayo kuhusu uzoefu waliopata wakiwa na sisi.

Wanafunzi wawili wa udaktari kutoka Ujerumani wakiwa na GreenVit Health kwa wiki moja katika afya ya jamii huko Moshi.

aTulifika Kama Wageni, Tukaondoka Tukiwa Sehemu ya Timu

Safari ya wanafunzi wawili wa udaktari kutoka Ujerumani kuja Moshi ilikuwa zaidi ya ziara ya masomo. Ilikuwa fursa ya kuelewa mfumo wa afya wa Tanzania, kujifunza kutoka kwa wataalamu wa afya, kushiriki katika huduma za afya ya jamii na kujenga mahusiano mapya kupitia uzoefu tuliopata pamoja na timu ya GreenVit Health.

Mwanzo wa safari na mapokezi ya kipekee

Kelvin aliratibu kwa umakini maandalizi ya safari yetu ya kuja Moshi, kuanzia kuwasiliana nasi tukiwa safarini hadi kutupokea, kutuandalia malazi mazuri na kutufanya tujihisi sehemu ya timu iliyotujali. Tulipowasili, tulipokelewa kwa ukarimu uliotufanya tujisikie tuko nyumbani.

Siku yetu ya kwanza ilianza kwa kutembelea ofisi za GreenVit, ambapo Kelvin alitueleza historia ya taasisi, jinsi inavyofanya kazi na miradi yake mbalimbali. Baadaye, Dkt. Arnold alitueleza kwa kina kuhusu mfumo wa huduma za afya nchini Tanzania, changamoto zake na nafasi ya magonjwa yasiyoambukiza katika afya ya jamii.

Mijadala hii ilitupa msingi muhimu wa kuelewa jinsi taasisi mbalimbali na ngazi tofauti za huduma za afya zinavyoshirikiana. Tulipata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni yetu na kujifunza kutokana na majibu na mijadala iliyofuata. Katika wiki nzima, tulihimizwa kushiriki kikamilifu, kuchangia mawazo na kujifunza kutokana na uzoefu wa timu.

Kujifunza kuhusu mfumo wa afya kupitia ziara katika vituo vya kutolea huduma za afya

Ili kuunganisha tulichojifunza na hali halisi ya utoaji wa huduma za afya, tulitembelea Kituo cha Afya Pasua tukiambatana na Dkt. Arnold. Kituo hicho kilikuwa na mazingira mazuri, yenye uoto wa kijani na majengo yanayohudumia mahitaji mbalimbali ya wagonjwa.

Dr Arnold akiwa na wegeni wetu Matilda (kushoto) na Anuschka (kulia) katika kituo cha afya Pasua

Tulitembelea maeneo kadhaa, yakiwemo jengo la huduma za watoto, chumba cha X-ray, famasia, maabara na chumba cha kujifungulia. Pia tulitambulishwa kwa baadhi ya watumishi na tulipata nafasi ya kujionea wenyewe changamoto zinazoweza kujitokeza katika utoaji wa huduma za afya katika ngazi hiyo.

Dkt Arnold akiwa pamoja na mmoja ya wageni wetu, Matilda katika famasi ya kituo cha afya Pasua

Ziara yetu iliendelea katika Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC), ambapo tulipata picha pana zaidi ya huduma zinazotolewa katika hospitali kubwa ya rufaa ya kanda. Tulitembelea idara na wodi mbalimbali, zikiwemo za macho; masikio, pua na koo; huduma za dharura; na matibabu ya saratani. Pia tuliona kitengo cha moyo, ambacho kilikuwa kikijengwa wakati wa ziara yetu.

Mbali na kutembelea maeneo ya kutolea huduma, tulitambulishwa kwa watumishi na wakuu wa idara mbalimbali, na tulikutana na wanafunzi wengine wa kimataifa waliokuwa wakipata mafunzo hospitalini hapo. Uzoefu huu ulitupa nafasi ya kuona kwa karibu wigo mpana wa huduma katika hospitali ya rufaa na mazingira ambamo wataalamu wa afya wanafanyia kazi.

Wakati wa ziara hiyo, pia tulihudhuria mhadhara wa Dkt. Howlett kuhusu ugonjwa wa konzo. Ilikuwa furaha ya kipekee kujifunza pamoja na wanafunzi wa Kitanzania na kuona jinsi mazingira ya pamoja ya kujifunza na kubadilishana maarifa yanavyoweza kuwaleta pamoja wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Afya Pamoja: Kujifunza kupitia huduma kwa jamii

Mojawapo ya matukio muhimu zaidi katika ziara yetu lilikuwa kushiriki katika programu ya Afya Pamoja inayoendeshwa na GreenVit Health.

Siku moja kabla ya tukio, tulitembelea ofisi za GreenVit Health kwa ajili ya maandalizi. Tulishirikiana na timu kuandaa vifaa, fomu na mahitaji mengine, ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa utaratibu mzuri.

Siku ya tukio, tulisafiri hadi kijiji kimoja huko Moshi ambako huduma za Afya Pamoja zilikuwa zikitolewa. Shughuli ilianza kwa utambulisho uliofanywa na Kelvin na sala, kisha usajili wa washiriki na kuanza kwa upimaji.

Tulishiriki katika kupima shinikizo la damu, tukifanya kazi bega kwa bega na madaktari waliokuwepo katika kuwahudumia wanajamii. Shinikizo la damu lilipimwa mara mbili. Baada ya hapo, washiriki walielekezwa kupima kiwango cha sukari mwilini, urefu na uzito. Huduma hizi zilitolewa na wanatimu wa GreenVit Health, wakiwemo Grace (Mama Chitema) na Goodluck.

Baada ya vipimo vya awali, Dkt. Arnold na Dkt. Pankras waliwahudumia wagonjwa, wakatoa matibabu yaliyohitajika na kuwapa baadhi yao rufaa kwa huduma zaidi pale ilipohitajika.

Huduma za Afya Pamoja hazikuishia kwenye upimaji na matibabu pekee. Jessica alitoa elimu kuhusu lishe bora, huku Kelvin akitoa elimu ya afya kwa washiriki na kujibu maswali yao. Jambo jingine la kuvutia lilikuwa kuwashirikisha wanajamii katika kujifunza jinsi ya kupima shinikizo la damu. Walipata nafasi ya kutumia vifaa hivyo wenyewe, na baadaye walipewa vifaa hivyo ili waendelee kuvitumia.

Elimu ikitolewa kwa washiriki katika shughuli ya upimaji, elimu hiyo inatolewa na Bwana Kelvin.

Kwetu sisi, hii ilikuwa mojawapo ya sehemu zenye maana kubwa zaidi katika ziara yetu. Kujionea wenyewe jinsi wanajamii walivyopata huduma, na kuona baadhi ya watu wakiwa na viwango vya juu vya shinikizo la damu, kulitufanya tutafakari kwa kina zaidi umuhimu wa programu kama hii.

Tulielewa kuwa Afya Pamoja haihusu tu upimaji na kugundua matatizo ya afya mapema, bali pia kuwapa watu maarifa na uwezo wa kushiriki katika kulinda afya zao wenyewe. Elimu ya afya, upimaji wa mara kwa mara na kuchukua hatua mapema vyote vina nafasi muhimu katika kuzuia au kupunguza madhara yanayosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.

Katika mazungumzo yetu, Dkt. Arnold alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kinga, hasa katika mazingira yenye rasilimali chache ambapo kutibu matatizo ya afya kunaweza kuwa na changamoto kubwa. Pia alieleza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa kinga na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza katika mifumo ya sasa ya huduma za afya.

Picha ya Pamoja baada ya shughuli ya upimaji, pichani (kuanzia kushoto) ni Pankrasi, Goodluck, Kelvin, Matti, Anuschka, Arnold, Jesca, Mama Chitema

Uzoefu huu ulituonyesha kwa vitendo jinsi huduma za afya ya jamii zinavyoweza kuunganisha upimaji wa mapema, elimu ya afya na ushiriki wa jamii. Ingawa siku ilikuwa ndefu na yenye uchovu, tuliondoka tukiwa na maarifa mapya na uelewa mpana zaidi wa kazi inayofanywa na GreenVit Health.

Zaidi ya kujifunza: Kufurahia Moshi na kujenga mahusiano

Mbali na shughuli za kitaaluma, safari yetu ilitupa nafasi ya kuifahamu Moshi na kufurahia mandhari yake. Tulitembelea chemchemi za maji moto, ambapo tulifurahia mandhari ya asili, tukaona samaki, tukaogelea na kupumzika baada ya siku zenye shughuli nyingi.

Katikati mwa wiki nzima ya kufanya kazi tulipata muda wa kuburudika katika chemchemi za Chemka.

Vilevile, tulishiriki milo ya mchana na ya jioni pamoja na timu ya GreenVit Health katika siku tulizokuwa Moshi. Zaidi ya kuwa nyakati za kula tu, nyakati hizi zilitupa nafasi ya kuzungumza, kufahamiana zaidi na kujenga mahusiano nje ya mazingira ya kazi. Pia tulipata nafasi ya kuuzunguka mji wa Moshi na kufanya manunuzi katika soko la mitumba la Memorial.

Tulipata muda kutembelea kanisa la kihistoria la Katoliki la Kibosho, lililojengwa mwaka 1893 na wajerumani.

Shughuli hizi zilitukumbusha kuwa kubadilishana uzoefu hakufanyiki hospitalini, ofisini au kwenye vikao pekee. Wakati mwingine, mazungumzo ya kawaida, matembezi na shughuli tunazofanya pamoja hujenga uelewano na mahusiano yanayoufanya uzoefu wa kujifunza kuwa wa kipekee zaidi.

Green Day: Kutafakari safari na kumbukumbu tulizojenga

Siku yetu ya mwisho ilikuwa na shughuli maalumu ya Green Day, iliyotupa nafasi ya kutembea pamoja, kuzungumza na kubadilishana uzoefu katika mazingira tulivu.

Baada ya matembezi, tulikula chakula cha mchana pamoja na kucheza karata. Ilikuwa nafasi ya kufurahia muda wetu pamoja na kuimarisha urafiki uliojengwa katika kipindi chote cha ziara.

Kila mmoja wetu alipata nafasi ya kueleza kilichomgusa zaidi katika wiki hiyo na kutafakari kumbukumbu tulizojenga pamoja. Kupitia mazungumzo haya, tulitambua jinsi uzoefu wetu ulivyotofautiana na kukamilishana, kuanzia kujifunza kuhusu mfumo wa afya hadi kushiriki katika huduma za jamii na kufurahia ukarimu wa wenyeji wetu.

Baada ya shughuli hizi, muda wa kuagana ulifika. Kelvin alitusindikiza hadi kituo cha mabasi kwa ajili ya safari yetu ya kurudi. Haikuwa rahisi kuagana baada ya wiki iliyojaa uzoefu na mahusiano mazuri, lakini tulibaki na shukrani kwa muda tuliokaa pamoja na ukarimu tulioonyeshwa na timu ya GreenVit Health.

Kumbukumbu na maarifa yatakayodumu nasi

Wiki tuliyokaa Moshi ilikuwa safari ya kujifunza kwa namna nyingi. Tulipata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu mfumo wa afya wa Tanzania, kuona jinsi huduma zinavyotolewa katika ngazi mbalimbali, kushiriki katika shughuli za afya ya jamii na kuelewa umuhimu wa kinga, ugunduzi wa mapema na elimu ya afya.

Zaidi ya maarifa ya kitaaluma, tuliondoka na kumbukumbu za ushirikiano, urafiki na ukarimu. Tunathamini fursa tuliyopewa ya kujifunza pamoja na timu ya GreenVit Health, na tunatumaini kuwa uzoefu huu utakuwa msingi wa mahusiano ya baadaye na fursa zaidi za kubadilishana maarifa.

Moshi ilitupokea kama wageni, lakini kwa muda wote tuliokuwa huko, tulijihisi sehemu ya timu. Na tulipoondoka, hatukuondoka na kumbukumbu pekee, bali pia na uelewa mpana zaidi wa maana ya kuunganisha maarifa ya kitabibu na mahitaji halisi ya jamii.

 

Subscribing you to our health tips...

Endelea Kupata Habari

Pokea vidokezo vya afya na maarifa ya hivi karibuni kwenye sanduku lako la barua pepe.

Tunaheshimu faragha yako na hatutashiriki anwani yako ya barua pepe.